Umuhimu wa kusoma vitabu
Kusoma vitabu limekuwa ni jambo gumu kwa wengi. Wengi wanashindwa, wachache wanajivuta vuta kusoma bila kumaliza vitabu walivyoanza kusoma na wachache kabisa wanaweza kusoma vitabu na kufaidika na maarifa yake.
Emmanuel Minga ni mwandishi na msomaji mzuri wa vitabu, ameandika mambo machache yafuatayo kugusia umuhimu wa kusoma vitabu.
Mtu mmoja aliwahi kusema ukitaka kumficha muafrika siri asiijue maisha yake yote basi iweke katika kitabu, lakini leo nataka nikuonyeshe vito vya thamani utakavyovipata pale tu ukijijengea tabia ya kusoma vitabu.
- Ndimo yalimo majibu ya maswali mengi unayojiuliza leo, maswali ya watu wengi mfano nifanyeje ili nifanikiwe kiuchumi, kiroho, mahusiano ,siasa n.k yote hayo yanapatikana kwenye kurasa za kitabu
- Utafunuliwa dunia ambayo hukuwahi kuijua. Ukitaka kujifunza hata vitu ambavyo hukuwahi kujifunza shuleni au kwa wazazi wako basi utajifunza kitabuni
- Itakusaidia kunoa shoka ambalo utalitumia kuangusha msitu mnene uliosimama mbele yako uzuie safari yako, ukitaka kujifunza namna na mbinu za kupambana katika maisha basi utazikuta kitabuni.
- Ndimo ulimolala ubunifu na vipaji vya kila aina, ukitaka kuwa mbunifu au kunoa kipaji chako basi pitia kurasa za vitabu.
- Ndimo ilimojificha furaha na kicheko, ukitaka uburudishe ubongo na kutunza maisha ya furaha basi jua kusoma vitabu.
- Vitakupa macho kuona katika giza ambalo wengine hawaoni, ukitaka kuwa na jicho la tatu kuona fursa kabla ya wengine basi jitahidi kusoma vitabu!.
- Vitakupa sababu ya kila kitu kwanini kipo na kina maana gani kwako, ukitaka kujua hilo soma kitabu.
- Ndimo ilimojaa hekima ya maisha, ukitaka kufanikiwa kimaisha soma vitabu.
- Ukiwa msomaji basi wewe ni kiongozi unayewaongoza wengine, kwa sababu unaujua mwelekeo (unayo dira). Utakuwa mtu usiyezuilika na itakufanya upae uishi katika ulimwengu wako mwenyewe uliojaa mafanikio, hamasa, ushindi na furaha.
- Vitakufanya uwe nguri na mtatuzi wa matatizo na changamoto zinazokukabiri wewe na jamii inayokuzunguka. Haya yote unayapata ukiwa Msomaji wa vitabu.
Hayo ni machache tu ila zipo faida nyingi mno zilizojificha katika kurasa za vitabu, anza kusoma sasa. Usiache kujifunza.
Imeandikwa na Emmanuel Minga na kupitiwa na DL Bookstore
Unataka kuanza safari ya kusoma vitabu sasa? Angalia vitabu vingi katika dukaletu la mtandao hapa au hapa.
Karibu
kwa maoni yako hapa chini.