Ishara tatu kwamba wasomaji hawamalizi kusoma kitabu chako
Si kila msomaji anayenunua kitabu atakisoma, wengine wanasoma kidogo tu, na wengine hawasomi kabisa. Lakini si waandishi wengi hufahamu jambo hili, furaha yao huwa “nimeuza kitabu, nimeingiza hela”. Kwenye tasnia ya uandishi, kuingiza pesa pekee si lengo la mwisho, kuona kwamba wasomaji wameelemika na wameburudika baada ya kusoma kitabu chako si jambo la kupuuzwa wala kupungunguzwa uzito wake.
Nikuulize ndugu mwandishi, Je! Wewe huwa unajuaje kama msomaji aliyenunua kitabu chako amekisoma na kukimaliza?. Kama majibu unayo ni vizuri sana, ila kama huna, basi nataka kukupa ishara tatu ambazo zitakusaidia kujua kama kitabu chako kimesomwa na msomaji amekimaliza.
1. Wamenunua wengi ila mrejesho wao sifuri. Kama umeuza nakala nyingi sana ila hupati maoni ya wasomaji wako, wakakwambia kitabu chako kimewasaidiaje kwenye maisha yao, basi ni ishara kwamba wananunua tu ila hawamalizi kukisoma au hawakisomi kabisa. Kama mwandishi una kiu ya kutaka kujua kama wasomaji wanasoma na kumaliza kitabu chako, waombe wakupe review, usikae tu bila kufanya hivyo. Mbali ya kwamba, kupata mrejesho sifuri inaonesha wasomaji hawamalizi kusoma kitabu chako, inaweza kukupa signal pengine kitabu chako ni kibaya
2. Kwa wanaoandika riwaya kwa mfumo wa series, ikiwa riwaya ya kwanza kwenye series inauza halafu riwaya inayofuata kwenye series haiuzi ni ishara kwamba riwaya yako haisomwi au wasomaji hawamalizi kusoma kwa sababu kama wasomaji wanasoma na kumaliza LAZIMA watataka kujua visa vinaendeleaje kwenye riwaya inayofuata.
3. Ukiacha tu kutangaza kitabu, basi mauzo ya kitabu yanarudi sifuri, hakuna unachouza. Pamoja na kwamba usipotangaza kitabu chako, wasomaji hawatakifahamu na kukinunua lakini mara unapoacha kutangaza na mambo yote yanarudi sifuri ni ishara kwamba kitabu chako wasomaji hawamalizi kukisoma. Kwa nini nasema hivi?, Kwa sababu, kuna word of mouth ambayo kama kitabu chako kinasomwa itaendelea kwa wasomaji na hivyo mauzo ya kitabu hayatashuka ghafla mpaka sifuri. Msomaji huyu atamwambia huyu na yule kuhusu kitabu chako na hivyo kitaendelea kuuza hata kama hukitangazi!.
Ni ishara ipi kati ya hizi inaonesha kitabu chako hakisomwi au wasomaji hawamalizi kukisoma? Nikupe nyongeza kidogo, ongeza maarifa na ujuzi zaidi wa kuuza kitabu kwa kusoma kozi hizi mbili
- Sanaa ya uuzaji wa vitabu. Hii ni kozi ya siku 8. Isome hapa
- Njia tatu za kuuza kitabu zilizo thibitishwa kuleta matokeo. Hii ni kozi ya siku 9. Isome hapa
Usiache kutuachia maoni yako kwenye comment hapa chini.
Karibu.