Njia tatu (3) za kumnasa msomaji asome kitabu chako
Kitabu kinaandikwa ili kisomwe lakini si rahisi kumnasa msomaji akasoma kitabu chako bila kukiacha hata akakimaliza. Unavyokianza kitabu chako ndiyo jambo muhimu zaidi kwa sababu hakuna msomaji atasoma sentensi inayofuata, kisha inayofuata na inayofuata kama sentensi ya kwanza haikumfanya kuvutika kusoma zaidi.
Kama mwandishi akifanikiwa kumfanya msomaji kutaka kujua zaidi,
akamjengea hamu ya kuendelea kusoma alichoandika, basi atakuwa
amemnasa msomaji kusoma kitabu chake chote. Huu ndiyo ujuzi ambao
kila mwandishi anatakiwa kuupalilia na kuujenga.
Kitabu kinachomnasa msomaji kinajibu maswali manne ya msingi ambayo msomaji wako atajiuliza
Je! kitabu hiki kitanifaa?
Ni nini nitajifunza?
Kitanisaidiaje?
Nitakifurahia?
Sasa,
Kuna njia nyingi za kuandika sumaku ya kumnasa msomaji asome kitabu, katika hizo nyingi tuone njia tatu
1. Toa kisa/stori inayoragbisha.
Unajua kwamba watu hupenda visa vyenye mvuto?. Stori inayoragbisha msomaji huamsha udadisi wake na hutaka kujua kisa kiliendeleaje, nini kilitokea na kadhalika.
Hivyo basi, kuandika kisa chenye mvuto kwa msomaji ni sumaku ya kumnasa msomaji akisome kitabu chako bila kukiweka chini mpaka akimalize.
Fikiria kisa kinachoanza na maneno haya;
“Tusingemuua mke wake” alisema mmoja ya wale wauaji, wakikipita kichaka alichojificha Albert – Kutoka kwenye kitabu cha IT CAN’T BE TRUE cha John Mwakyusa, kama msomaji lazima utavutika kutaka kujua nini kiliendelea kwenye tukio hili.
Kutoa stori inayomragbisha msomaji ni njia ya kwanza maarufu sana ya kumnasa msomaji asome kitabu chako.
2. Uliza swali la kumshurutisha msomaji.
Kuuliza swali ni njia nyingine ya kumnasa msomaji asome kitabu chako kwa sababu msomaji atajaribu kujibu swali lako. Si hivyo tu, pia inamfanya msomaji apate hamu ya kutaka kujua wewe mwandishi ulijibuje swali ulilouliza.
Fikiria kitabu kinachoanza na swali kama hili;
“Wale wauaji kumi walifungiwa ndani ya chumba kimoja. Ghafla aliingia mtu mmoja aliyeficha uso wake na kumuua muuaji mmoja. Je kulikuwa na jumla ya wauaji wangapi?. Mwalimu wa Hisabati alianza na swali hili kabla ya kuanza kufundisha, ukimya ulipita bila majibu. Pengine hii ndiyo ilikuwa sababu sikulipenda somo la Hisabati, hivi kama ingekuwa ni wewe ungejibu nini?”
Je wewe hungeshawishika kujibu swali hili kiasi cha kukufanya uendele kusoma kitabu?.
AD: Unapata changamoto kuuza kitabu chako? Mwarobaini umepatikana! Soma kozi ya Njia tatu za kuuza kitabu chako zilizo thibitishwa kuleta matokeo. Jisajili hapa →
3. Weka utafiti.
Wasomaji wanapenda data za utafiti, ni kitu kinachowavuta wakisome kitabu. Kwa hiyo, anza kitabu chako cha kuweka data za utafiti na itakuwa ndiyo sumaku yako ya kumnasa msomaji akisome kitabu
Kwa mfano, kitabu kinachoanza kwa data kama hivi, kitamvutia msomaji kukisoma;
“Zaidi ya 80% ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 – 25 wanapenda picha na video zenye maudhui ya ngono kwenye mitandao ya kijamii. Zipo sababu nyingi zinazosababisha jambo hili na kitabu hiki kinalenga kukupa data kutoka kwenye utafiti uliofanyika tangu mwaka 2018 – 2023”
Utafiti ni sumaku nyingine ya kutumia unapoandika kitabu chako ambayo itamnasa msomaji akisome kitabu chako mpaka mwisho.
Umejifunza nini kwenye chapisho hili? Karibu kwa maoni hapa chini.