"0" Mileage: Usiolewe kabla hujaolewa
Nakumbuka siku moja nilikuwa nafanya mizunguko yangu ya kawaida, nikitoka eneo linaloitwa Leganga lililopo Mji wa Usa-River kuelekea Arusha Mjini. Kwenye usafiri wa DALADALA niliokuwa nikitumia kwa siku hiyo, ghafla kulizuka mada ambayo naomba niipe kichwa cha SHUKA JEUPE. Dereva wa daladala ambaye ni kijana wa kati ya umri wa miaka 25 hadi 30, alianza kurushiana maneno na mama mmoja wa makamo ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo hizi za masokoni. Mama alikuwa akimsisitiza dereva juu ya kuoa, kwa kuhamaki dereva akaanza kulalamika, akisema siku hizi hakuna wasichana tena wakuoa kama ilivyokuwa zamani. Na akaendelea kusema kwamba zamani binti alikuwa akiolewa shuka jeupe linawekwa kitandani ule usiku baada ya harusi, na kilichokuwa kinategemewa pale ni asubuhi shuka kukutwa limelowa damu. Damu ni ishara kwamba yule binti alikutwa ni mwanamwali au bikira, yaani hakuwahi kumjua (kulala/kushiriki tendo la ndoa) na mwanaume yeyote kabla ya yule aliyemuoa.
Basi hapo sasa na abiria wengine walianza kupokelea kwa maneno mengi sana hiyo mada, wengi sana walionyesha masikitiko yao juu ya hali inayoendelea sasa kwenye jamii ya leo. Wasichana wengi wamekosa thamani kwa kuwa wameshindwa kujiheshimu na kujitunza, wengi wamekuwa wepesi KUOLEWA kabla HAWAJAOLEWA, namaanisha wamekuwa tayari bila aibu kuwahudumia wavulana walionao kwenye mahusiano huduma zote za ndani ya ndoa kabla hawajaolewa. Wamekuwa WAKE ambao bado hawajarasimishwa, wanajitutumua kutoa huduma ambazo wakati wake haujafika. LIKO WAPI SHUKA JEUPE LEO?, inatia huzuni sana kuona heshima, thamani na ubora wa msichana ukipotea kisa ni kujirahisisha.
Nilipofika ninapotakiwa kushuka, nilishuka lakini kichwani niliendelea kujiuliza maswali mengi sana. KWANINI kwenye zama zetu hizi SHUKA JEUPE hakuna tena?, Tunakosea wapi? na kwanini TUNAKOSEA?.