Barua kwa binti
Kwako Binti,
Ni matumaini yangu kuwa u mzima na Mungu amekujaalia uhai na nafasi ya kujifunza kama hivi kupitia kurasa za waraka huu, lakini kwa wale ambao si wazima au wanachangamoto mbalimbali, nichukue fursa hii pia kukufikia kwa pole na kukuombea Mungu ahusike na jambo lako.
Natambua mambo ni mengi na muda pengine hautoshelezi kuyasema yote, lakini asante kwa kuchagua kujifunza maana elimu haina mwisho, na wakati mwingine elimu bora zaidi huja kwa njia isiyo rasmi.
Ujumbe huu ni shauku kubwa ya moyo wangu kuzungumza na wewe binti, kwasababu kuna nyakati katika maisha ambazo nami pia nilikua binti kama wewe, na nikiangalia nyuma nilikopita, kuna mambo ambayo sitamani binti mwigine apitie huko nilikopita na mengine bora zaidi ambayo natamani uyapitie kwaajili ya maisha yako.
Nimekua na shauku hii ya kuzungumza na wewe binti nikiamini sio mimi tu peke yangu bali wako wengi ambao wangetamani kuzungumza na wewe lakini huenda hawana nafasi kama hii ya kukufikishia ujumbe, ila naamini mara usomapo ujumbe huu utatusemea wengi na utapata nafasi ya kumshirikisha binti mwingine pia kwaajili ya kugusa maisha ya mabinti wengi zaidi.
Nikukumbushe tu, huenda yaliyo humu ndani mengi ukawa unayafahamu, nikupongeze kwa hilo, na huenda mengi pia usiyafahamu kwa namna yalivyoletwa kwako, au pia huenda ukatamani kusikia mengi ambayo humu hayamo, nikutie moyo tu, waraka huu sio mwisho wa elimu yote ya binti na wala sio kila kitu, bado tutaendelea kujifunza kila mara tunapopata upenyo.
Lengo kuu ni kumtia moyo binti, kumsaidia kufika zaidi ya alipofika, na kumshika mkono kumvuta upande wa pili wa ndoto zake.
Kitabu hiki cha "Barua Kwa Binti", kikawe chachu kwako na kwa binti mwingine popote alipo, kikakuwezeshe sio tu kuota ndoto kubwa, bali kuzifikia ndoto hizo kwa wepesi na ubora zaidi ya mimi au sisi tuliotangulia.
Kila la kheri katika kuzipambania ndoto zako, hauko peke yako, na nitafurahi kusikia toka kwako kwa mawasiliano ndani ya kitabu hiki.
Wenye hekima wanasema, maji ukishayavulia nguo sharti uyaoge. Msemo huu mimi hupenda kuuita kama msemo wa sharti, yaani iwe isiwe lazima iwe.
Sasa maadam umeshika kitabu hiki pia, nikuombe usichokee njiani, tuendelee pamoja kujifunza kupitia waraka huu kwa binti ambao ninaamini utayabadilisha maisha yako na kukupa nguvu zaidi ya kuinuka tena.
Asante kwa kuutenga muda wako kukutana nami kupitia kurasa za kitabu hiki, ninafuraha kubwa kuwa sehemu ya muda wako leo.
"Barua Kwa Binti" ni ujumbe ambao natamani sana kuufikisha kwako, "BINTI", ujumbe ambao ukiuelewa, huenda ukakufaa sana katika maisha yako, ujumbe ambao binafsi sikupata pengine bahati ya kuusikia nikiwa kama wewe na pengine nilijifunza mengi mwenyewe kwa kadri nilivyokua nikikua.
Ninatambua yako mambo mengi ambayo umeyasikia, na hasa ukizingatia ni ulimwengu wa teknolojia, au pengine wewe unabahati ya kuwa na waalimu wengi waliokuzunguka, lakini naamini bado iko nafasi ya kujifunza, maana ambapo hukupita yupo anaepitia hapo na kujifunza toka kwake si ujinga.
Niendelee kukukaribisha sana, ikiwa unapitia mengine magumu, usikate tamaa, hauko peke yako na wala wewe sio wa kwanza.
Karibu sana katika kuisoma barua hii, barua yenye mafunzo mengi, barua yenye kukukumbusha vingi na barua yenye kukutia moyo katika safari yako ya kuzifikia ndoto zako bila kujali ukubwa wa ndoto hiyo.
Asante kwa kutenga muda na karibu tuendelee, utajifunza mengi yakiwemo:Kujitambua, Kujithamini, Kujiamini, Hedhi Salama, Mahusiano, Namna ya kusimama tena mara unapokua uko chini au umekutwa na ambayo hukutegemea, Jinsi ya kuzipambania ndoto zako na mengine mengi.
Nikutakie kheri na mafanikio unapojifunza nami na ninaimani hautabakia kama ulivyo kuwa.
Endelea kufanikiwa.