Nguvu ya Fikra
Hakuna kitu chenye nguvu duniani kinachoweza kubadili maisha ya mwanadamu kama fikra; Fikra ni chimbo la mabadiliko, fikra ndio mwanzo wa maendeleo. Fikra iliyonyooka inaweza kubadili uwanja wa vita kuwa uwanja wa amani, fikra iliyonyooka inaweza kufanya paradiso ikashuka duniani.
Kwanini nasema hivi? Kwa sababu tangu nianze kujifunza elimu ya maendeleo binafsi nimegundua kuwa mabadiliko yoyote chanya iwe kwa mtu binafsi au jamii yanaletwa na fikra. Wote waliowahi kufanya mabadiliko makubwa na chanya kwao binafsi au kwa jamii walitumia NGUVU YA FIKRA zao na ndipo wakapata matokeo hayo makubwa.
Hebu jiulize wewe unatumiaje fikra zako? Dennis Mpagaze aliwahi kusema fikra zetu zimevaa nepi, uongozi wetu umevaa nepi, wasomi wetu wamevaa nepi, na taifa letu limevaa nepi..
Akiwa na maana ya kwamba fikra zetu bado ni changa, tunashindwa kutumia nguvu ya fikra zetu kufanya mabadiliko, kiasi ya kwamba kila kitu tunategemea kufanyiwa.