Njia za kukustawisha kiuchumi
Mafanikio ya kiuchumi ni mchakato unaohitaji uwekezaji wa nguvu, juhudi na ufahamu (akili). Kustawi kiuchumi sio uyoga, inahitaji uwajibikaji, uvumilivu na subira kufikia viwango vikubwa vya mafanikio. Hakuna ustawi usio na gharama. Kama vile huwezi kuokota gari au nyumba, huwezi kufanikiwa bila kuwajibika. Kustawi kiuchumi kunaanza na kufahamu kwamba ni mpango wa Mungu kila mwana wa Mungu kufanikiwa na kumiliki uchumi.
Kumbukumbu 8:18
“Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”
Mungu hawezi kukupa nguvu ya kupata utajiri kama hataki uwe tajiri, na katika agano la wokovu, uchumi ni sehemu mojawapo ambayo Yesu alilipa gharama. Wengi tunabaki maskini kwa kufikiri wokovu ni wa roho zetu ili kwenda mbinguni tu bila kutambua wokovu ni uzima kuanzia rohoni mpaka mwilini. Umaskini siyo sehemu ya maisha ya yeyote aliyezaliwa mara ya pili. Kazi ya msalaba ilikomboa mpaka uchumi wako ili usiishi kimaskini.
2 Wakorintho 8:9
“Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”
Wana wa Mungu kuishi maisha ya kimaskini ni aibu. Gharama ya utajiri wa kila anayemwamini Yesu Kristo ilishalipwa na Yesu mwenyewe. Ni jambo la kuchukua hatua na kuingiza ufahamu katika matendo tu na kuanza kuishi maisha ya ustawi.
Changamoto tuliyo nayo wengi ni mafundisho yasiyo sahihi juu ya maisha ya utauwa na kumiliki uchumi. Wengi wamefundishwa kuwa fedha ni shina la mabaya wakati Biblia inachokataza ni kupenda fedha (1 Timotheo 6:10). Kuna watu Mungu aliwatajirisha sana na bado wakamtumikia Mungu kwa unyenyekevu wote. Ibrahimu na Ayubu walikuwa matajiri wakubwa na bado wakampendeza Mungu kwa viwango vya juu.
Ni mpango wa Mungu wewe kutajirika. Ni mpango wa Mungu wewe ustawi sana sana kiuchumi. Uchumi ni nyenzo muhimu sana katika ufalme wa Mungu. Kuna viwango hutaweza kufika vya kumtumikia Mungu hata kama una upako mkubwa kiasi gani kama huna nguvu ya kiuchumi.
Katika kitabu hiki utajifunza njia chache za muhimu sana ili kukuwezesha kustawi kiuchumi. Haijalishi umezaliwa familia ya aina gani, haijalishi una elimu au huna, ukiamua inawezekana. HAKUNA JAMBO LINALOMSHINDA ALIYEKUSUDIA NA KUAMUA KUCHUKUA HATUA. Kiwango chako cha kufanikiwa na kustawi kiuchumi kinaamuliwa na wewe. Haijalishi utakutana na upinzani kiasi gani, PENYE NIA PANA NJIA. Kataa umaskini, chukia umaskini, Mungu yuko tayari kukustawisha.