Eden University of Management (Swahili version)
Watu wengi tukisikia Edeni picha ya kwanza inayotujia ni maua, miti na majani. upande mwingine zinakuja picha za wanyama mbalimbali akiwemo na nyoka aliyesababisha anguko ambalo mpaka sasa limetuletea shida kubwa.
Picha nyingine inayokuja kutoka Edeni ni kutupiana lawama kulikoanzia kwa Adamu mwenyewe kwenda kwa mkewe Eva, kutoka kwa Eva kwenda kwa nyoka ambaye anaonekana kama ndiye chanzo cha matatizo yote pale bustanini.
Mkazo mdogo sana umewekwa na walimu mbalimbali kuhusu hasa Mungu alitaka nini kizaliwe Edeni, lengo na madhumuni ya Mungu nyuma ya kuitengeneza Edeni hasa yalikuwa ni nini? Mungu aliumba Dunia kubwa sana, lakini ni kwa nini aanze na kumuweka mwanAdamu katika kasehemu kadogo tu kalikoitwa Edeni, kwa nini asimuache azurure atakavyo angali dunia ni kubwa kiasi cha kutosha? Afanye jambo lolote analojisikia? kwa nini amuwekee mipaka, ampangie majukumu, amuwekee na msaidizi. Kikubwa kuliko vyote ampe maelekezo ya kuishi humo, maana yake bila hayo maelekezo hata kama Edeni ina kila kitu anachohitaji mwanAdamu bado ingemuwia ngumu sana kufanikiwa pasipo kufuata maelekezo ama kupitia mafunzo hayo.
Yapo makusudio ambayo Mungu alikuwa nayo kichwani kabla hata hajatengeneza bustani ile, kuna vitu vilimsukuma kuitengeneza na kumuweka mwanAdamu ndani yake. Lipo kusudi ambalo alitamani MwanAdamu alifikie duniani lakini ni baada ya kupita katika mafunzo maalumu aliyoyaandaa ndani ya bustani ya Edeni. Kupitia kitabu hiki, ndugu msomaji, utakwenda kuyaona mambo hayo na kuyaelewa katika mapana makubwa zaidi ili kuweza kuinua uelewa wako, huenda hata sasa uko ndani ya Chuo Kikuu cha Edeni huku upande mwingine ukimlaumu Adamu kwa yale ambayo alishindwa kuyatekeleza kumbe nawe ndiyo hayo hayo unapaswa kuyafanya sasa na huna ufahamu.
Kama ambavyo tunaona katika vyuo vyetu vya leo, ndivyo na Edeni ilikuwa. Mkufunzi Mkuu alikuwa ni Mungu mwenyewe, Chuo kilikuwa na maelekezo ambayo Adamu alipatiwa mara tu alipowekwa, mafunzo yalikuwa ya nadharia na vitendo. Alipata nafasi ya kuonesha uwezo wake akiwa chini ya Uongozi wa Mkufunzi Mkuu ambaye ndiye Mungu mwenyewe. Kama ambavyo ilivyo katika siku za leo, hakuna shule isiyo na mitihani, mtihani wa nyoka tunaoukumbuka zaidi haukuwa wa kwanza. Adamu alipitia mitihani kadhaa akiwa ndani ya Edeni na mingi aliivuka kwa kufanya vizuri sana. Maisha ya ADAMU ndani ya Chuo kile yamejaa mafunzo adhimu ambayo yanaweza kutufaa katika siku zetu hizi za leo ili kuboresha namna tunavyoishi.
Ni maombi na dua zangu, pindi utakapomaliza kusoma kitabu hiki ukawe na uelewa kamili wa nyakati na majira ya maisha yako, ukaitumie vema Edeni yako na hatimaye ufike kule ambapo Mungu amekukusudia ufike, ufanye yale aliyokusudia ufanye na uwe yuleyule ambaye alikuumba na kukukusudia uwe. kupitia maarifa sahihi ndipo utaweza kuinuka na kusimama katika nafasi yako na mwishowe kuzaa matunda ambayo yatakuwa na faida si kwako tu bali hata jamii inayokuzunguka.
Recommended for you


