Ndoa si Ndoano
Kitabu hiki kitakupa wewe UELEWA wa mahusiano ya ndoa, ambayo ni nguzo muhimu sana kwenye maisha ya mahusiano. Hebu pata picha, kama unauelewa wa jinsi gari lako linavyofanya kazi, hata likipata hitilafu ukiwa safarini ni rahisi kuitatua hitilafu hiyo hata kama itakuwa imekupata porini. Huta kasirika na kulitukana gari kwa hasira, bali utaanza kulitatua tatizo lililojitokeza.
Kama unataka kuwa na ndoa bora, yenye furaha, amani na kudumu basi unatakiwa uwekeze kwenye uelewa. Uelewa juu yako wewe, juu ya mtu unayehusiana naye, lakini pia uelewa wa mahusiano ya ndoa. Unapaswa kuelewa mahitaji ya mwenza wako, matarajio yake kwako, na ndoa kwa ujumla, na ndiyo sababu ya uwepo wa kitabu hiki.
Kitabu hiki kina kupa uelewa kwamba upendo pekee haufanyi ndoa kudumu bali kanuni ya maarifa, uelewa na hekima. Ili ndoa isiwe ndoano kwako, maarifa, uelewa na hekima utakayojifunza kwenye kitabu hiki yatafanya ndoa yako isiwe ndoano.
Utajifunza pia kanuni ya utayari na sababu muhimu za kukufanya uingie kwenye ndoa na mwenza wako na namna bora ya kuendelea kuwa na ndoa yenye furaha, upendo na amani.
Na kama ulishaingia kwenye ndoa na mtu ambaye unaona hamuendani, utajifunza jinsi ya kutumia kanuni ya ushawishi ili mwenza wako huyo aweze kubadilika na siyo wewe kumbadilisha bali yeye mwenyewe kubadilika.
Si hivyo tu, utajifunza pia kanuni ya utofauti baina yako na mwenza wako na jinsi ya kuutumia utofauti wenu ili kuwa na ndoa yenye furaha na amani. Kanuni ya utofauti ndiyo huzaa kanuni ya mahitaji ambayo ni muhimu kuelewa mahitaji ya mwenza wako kwenye ndoa na kuweza kumtimizia huku na yeye akitimiza mahitaji yako pia. Migogoro mingi huwa inatokana na wanandoa wengi kutokujua mahitaji ya wenza wao, hivyo kushindwa kuyatimiza.
Utajifunza kanuni ya mahusiano ni mawasiliano ambayo ni nguzo muhimu ya mahusiano ya ndoa. Namna nzuri ya kuwasiliana na mwenza wako ili mahusiano yenu yaweze kuendelea kuimarika zaidi kila kunapoitwa leo.
Kitabu hiki pia kitakupa maarifa na uelewa juu ya kanuni ya haiba yako na ya mwenza wako na namna ya kuzitumia haiba zenu ili kudumisha mahusiano yenu ya ndoa. Bila kusahau, matumizi sahihi ya kanuni ya hisia kwenye ndoa yenu kwa kuongozwa na hisia ya furaha.
Karibu uendelee kupata maarifa haya.