Jilipe mwenyewe kwanza
Kitabu hiki cha JILIPE MWENYEWE KWANZA ni mwongozo sahihi wa kifedha kwa mtu yeyote anayetaka kujijengea uhuru wa kifedha na utajiri kwa kuanzia pale alipo sasa. Kama jina linavyojieleza, zoezi la kujilipa mwenyewe linapaswa kuwa la KWANZA. Yaani unapopokea kipato chako, kabla hujafanya matumizi yoyote, unaanza kwa kutenga pembeni fungu la kujilipa, halafu kinachobaki ndiyo unatumia.
Ni kwa kutumia kanuni hiyo ya KUJILIPA MWENYEWE KWANZA ndiyo unaweza kujilipa hata kama kipato chako ni kidogo kiasi gani. Unapoweka vipaumbele sahihi kwenye matumizi ya fedha zako, kwa kuanza na kujilipa, unaweza kutumia kipato kidogo ulichonacho kujenga utajiri mkubwa.
Neno utajiri limewatesa sana watu wengi. Watu wamehangaika na mambo mengi sana kupata utajiri. Wapo walioiba na kudhulumu wengine, na utajiri walioupata haukudumu. Wapo waliocheza bahati nasibu na kamari na wengi walikosa, huku wachache waliopata nao wakishindwa kudumu na utajiri. Na wapo waliotumia njia za kishirikina na bado wasipate utajiri unaodumu.
Mambo mengi kwenye maisha huwa ni rahisi, lakini watu huwa wanahangaika kuyafanya kuwa magumu. Ikiwepo swala la utajiri, mahangaiko yote ambayo watu wanayo juu ya utajiri, ni kujitesa tu. Kanuni ya kujenga utajiri ni rahisi na inayoeleweka na kila mtu. Na inasema hivi; MARA ZOTE MATUMIZI YAWE MADOGO KULIKO KIPATO CHAKO.
Kama utaamua kuachana na mambo mengine yote na ukaamua kukomaa na hilo moja tu, kwamba kwenye kila kipato unachoingiza matumizi yawe madogo kuliko kipato hicho na ukaenda hivyo kwa maisha yako yote, lazima utajenga utajiri.
Huo ni uhakika, siyo kubahatisha. Utawezaje kuhakikisha mara zote matumizi yanakuwa madogo kuliko kipato? Jibu lipo ndani ya kitabu hiki, kwa kuhakikisha kwenye kila kipato unachoingiza, unajilipa wewe mwenyewe kwanza kabla hujaanza matumizi. Na kile unachojilipa hukiachi kiholela, bali unakiweka kwenye gereza ambapo huwezi kukifikia kirahisi.
Yote hayo utajifunza kwa kina kwenye kitabu hiki. Na kipato chochote ambacho utakipata badala ya kufikiria kuwalipa wengine utaanza kujilipa wewe mwenyewe kwanza, badala ya kufikiria kulipa kodi, kununua nguo na vitu vingine.