Jipu ndani ya ubongo - Simulizi ya kweli
Naanza kuumwa nikidhani ni ugonjwa wa kawaida. Hospitali pia natibiwa magonjwa ya kawaida; Malaria, homa ya tumbo na maambukizi ya bakteria. Wiki tatu zinapita, nazidi kuumwa, kichwa, kutapika na mwili kuisha nguvu. Najaribu hospitali nyingine na kugundulika kuwa nina uvimbe. Ndio, uvimbe kwenye ubongo. Nauita JIPU, kwani umeshikamana na ubongo kama doa lilivyo kwenye nguo. Natakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka vinginevyo nitakufa ghafla. Daktari anamwambia mume wangu akubaliane na hatari iliyoko mbele yangu ya kupoteza kuona, kupooza, kupoteza kumbukumbu au kufa baada ya upasuaji. Godfrey, mume wangu, analazimika kufanya maamuzi yenye hatari kubwa kwa maisha yangu.
Nafsini
namuamini Mungu kuwa HAKUNA KITAKACHOPUNGUA, HAKUNA KITAKACHOVUNJIKA.
Hii siyo
hadithi, ni simulizi la kweli. Leo ni mwaka mmoja umepita, na mimi mwenyewe
nimeandika kitabu hiki, kuelezea ukuu wa Mungu awezaye kufufua hata waliokufa,
jinsi alivyotenda kwangu.