Mzimu wa Kichaa
Mzimu wa Kichaa ni kitabu chenye hadithi ya kubuni yenye mkusanyiko wa masimulizi yanayohusu ulimwengu wa kawaida wa maisha ya watu na ulimwengu usioonekana kwa macho ya kawaida. Riwaya hii ni ya kipekee kwa kuwa imezungumza mambo ambayo jamii nyingi haziyaweki wazi. Mambo ya uchawi na ushirikina yamefichwa sana, na watu wengi hawapendi kuyajadili kwa uwazi na undani. Mambo hayo yanathibitishwa kuwepo katika maandiko ya kiimani kama vile Koran na Biblia tangu karne na karne na jamii nyingi zinazungumza uwepo wa uchawi, ushirikina na majini.
Kitabu hiki kinasimulia kwa kina jinsi uchawi na ushirikina unavyoleta maumivu na huzuni kwa wanajamii wasio na hatia. Kuna simulizi na matukio ya aina mbalimbali ambayo huonekana ni ya kawaida au bahati mbaya katika jamii, lakini katika kitabu cha Mzimu wa Kichaa, utapata picha nyingine adimu usiyoijua kuhusu anga na mifumo ya ardhini, majini na chini ya bahari.
Kina mafundisho mengi ikiwa ni pamoja na mwenendo na tabia njema ya utu, upendo, ushirikiano na kutokukata tamaa. Miujiza mbalimbali iliyomo itakupa msisimko na kukufanya uelee katika tafakuri ya kina kuhusu maisha na matukio katika ulimwengu halisi na ule wa kimazingara. Utapata maarifa adimu ambayo hayazungumzwi kirahisi katika jamii. Utafurahi, utahuzunika, utashangaa, utakasirika, utatafakari na utapata pia ujasiri katika safari ya maisha yako.
Mtiririko wa masimulizi unakufanya kutaka kujua tukio litakalofuata, hivyo ukianza kusoma kitabu hiki, hutatamani kukiweka chini. Ni kitabu kinachoonesha uwepo wa mambo ya nuru na giza katika jamii, ambayo hasa kizazi cha sasa hakiyafahamu; mambo ya jadi na tamaduni za jamii. Nakuachia jukumu la kufanya uchambuzi wako pia baada ya kusoma kitabu hiki cha kusisimua.