Yusufu nina ndoto
Mtunzi wa kitabu hiki ni mwandishi maarufu wa vitabu vya mafanikio. Ujumbe wa kutafakarisha na kusisimua wa kitabu hiki ni kuwa, ukiwa na uwezo wa kuota ndoto bila kulala usingizi unakuwa na uwezo wa kubadili maisha yako. Ukibadili unachokiota unabadili unachokizalisha, unabadili maisha yako.
Mfano wa kuigwa wa muota ndoto ni Yusufu wa Agano la Kale. Ndoto yake ilizongwa na misukosuko. Ndugu zake waliomuonea wivu na kumuuza. Ndoto yake waliiwekea nukta, Mungu aliweka alama ya mkato. Mtunzi ameinakishi dhana ya ndoto kwa maneno ya kutia matumaini katika sura 39. Hata nyota ya ndoto yako ikipotea kama nyota ya Yusufu ilivyopotea ni MARUFUKU KUKATA TAMAA. Nyota ya ndoto itaonekana tena. Kuna mambo mengi ya kufanya kufanikisha ndoto. Anza na ulichonacho na anzia ulipo.
Ukitaka kutimiza ndoto zako lipa gharama za ndoto. Amka kabla ya ndege wa angani kuzitekeleza ndoto zako. Ili usipishane na ndoto zako hesabu baraka zako na si balaa. Ukiilinda afya yako, umeilinda ndoto yako. Ukiwa na ndoto usipige kelele, watu wataona matokeo ya ndoto zako.
Tofautisha ndoto zako na ndoto za watu wengine, kuwa wewe zaidi. Ukiwa na ndoto ambatana na watu wenye ndoto. Kaa na waridi unukie. Ng'ang'ania ndoto yako kama stampu kwenye bahasha. Nampongeza ndugu Edius Katamugora kwa kazi hii nzuri sana. Kitabu hiki Yusufu Nina Ndoto ni dira kwenye barabara ya mafanikio. Kisome hutajuta kwa nini umekinunua! (Padre Dkt. Faustin Kamugisha Mtunzi wa Kitabu Matatizo si Tatizo)