Ijue Sheria ya Ndoa, Mirathi na Uandaaji wa Wosia
Kitabu hiki kimejaa Maarifa na ufahamu wa kisheria juu ya taasisi muhimu ya ndoa. Kimechambua mambo mengi muhimu ambayo jamii kwa ujumla wake inapaswa kuyafahamu na kuyazingatia kwa maslahi mapana ya ustawi wa familia. Ukweli ni kwamba jamii kubwa ya Watanzania haina uelewa mkubwa kuhusu mambo mengi mtambuko yahusuyo ndoa, Wosia na Mirathi.
Watu wengi wamejikuta wakiingia kwenye ndoa pasipo kujua wajibu wa kisheria wanaoambatana nao katika ndoa. Na kwa kuwa hawajui sheria ya ndoa wamejikuta wakifanya uamuzi hasi ambao yamesababisha madhara makubwa mno kwenye familia zao ya ukatili wa ndoa kama vile vipigo, unyanyasaji wa kihisia, ulemavu, vifo na mengine mengi. Zipo baadhi ya tamaduni ambazo kitendo cha mume kumpiga mke kwao si kosa. Waathiriwa wa ukatili huu hasa wanawake, wengi wao hawajui wapi pa kukimbilia au kwenda kupata msaada wa kisheria. Kitabu hiki kimeeleza njia nzuri za kutatua migogoro na kuondosha tofauti za wanandoa pasipo kuathiri utu wa mtu.
Kwa upande mwingine, suala la Mirathi ni tatizo kubwa sana, kesi nyingi kwenye mahakama za mwanzo ni zile zinazohusu Mirathi. Watu hawana elimu ya kutosha na hawajui cha kufanya ili kulinda mali za marehemu zisilete mafarakano mara tu baada ya kifo chake. Wajane wengi wamedhulumiwa haki zao na wengine wamelazimika kukimbia nyumba zao ili kusalimisha maisha yao. Lakini hii yote ni kutokuwa na elimu ya sheria ya Mirathi. Kitabu hiki, aghalabu kimetoa elimu ya mirathi na kueleza hatua kwa hatua nini kifanyike ili kufanikisha usimamizi na ugawaji wa mali za marehemu kwa wanufaika. Hivyo, bila shaka kupitia kitabu hiki jamii itapata kujua jinsi ya kutatua changamoto za mambo ya mirathi.
Aidha, suala la kuandika au kuandaa wosia limetafsiriwa vibaya na watu wengi. Baadhi ya watu wanaamini kuwa kitendo cha mtu kuandika wosia ni kujitabiria kifo. Wazo hili huamsha hofu kwa wengi na ni dhana iliyosambaa kwa kasi kubwa na kuaminika hivyo na wengi. Si hivyo tu, lakini hata namna ya kuandika wosia wenye mashiko kisheria ni changamoto kwa watu wengi.
Mwandishi wa kitabu hiki amelezea vizuri sana mambo mengi yanayohusiana na wosia, jinsi ya kuandaa wosia, aina za wosia, faida za wosia na watu wanaoweza kuandika wosia wametajwa humu. Hivyo, kitabu hiki kinaweza kuwa ni msaada na suluhisho la utatuzi wa changamoto zinazoisumbua jamii kuhusu wosia. Mwandshi amelenga kuisaidia na kuielimisha jamii kutumia njia sahihi za kutatua changamoto na migogoro isiyo na lazima kwa watu wote wanaotamani kuacha mali zao zikitumika katika hali ya amani na usalama mara baada ya vifo vyao. mwandishi amekusudia kupeleka elimu kwa wanandoa jinsi ya kutekeleza majukumu na wajibu wao kwa lengo kuu la kuepusha ugomvi, malumbano na usaliti kwenye uhusiano ambao husababisha kupeana talaka na kuachana. Kwani suala la talaka na kuachana kwa wanandoa ilimesababisha usumbufu mkubwa kwenye malezi ya watoto pia kuacha maumivu makubwa ndani ya mioyo ya wanandoa, ukizingatia kuwa zipo sababu ambazo hutokana na kukosa ufahamu kwa nini kifanyike ili kusuluhisha jambo ambalo lingeweza kuepukika.
Soma kitabu hiki ili kulinda ndoa yako na kuepuka migogoro inayosababishwa na kutokujua sheria ya ndoa, wosia na mirathi. Mwandishi wa kitabu hiki ametumia lugha rahisi na inayoeleweka kwa watu wa kada zote hususani wale ambao siyo wanasheria.