Zijue nyakati na majira katika mpango wa Mungu
Kila zama na watu wake, kila nyakati na matendo yake, naam kila matendo ni matokeo ya mapokeo ya mafunzo na hekima walizonazo watu wa zama husika. Kama ningeliweza, ningelipaza sauti yangu isikike na watu wote waweze kusoma kitabu hiki. Kitabu hiki, “Zijue nyakati na Majira katika mpango wa Mungu”, kimenifanya nizidi kumshukuru Mungu kwa Baraka na Neema ya kutupa Mtumshi wake, Eng. Bujo Mwakapalila (Mwandishi) ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuilisha jamii Neno la Mungu na kuwapa watu kiu ya kutaka kula Mkate wa uzima.
Kitabu hiki kina sura Ishirini na mbili (22) ambazo zinatoa mafafanuzi kuanzia ‘Nyakati za wamataifa’ (Sura ya kwanza) hadi kufikia ‘Mambo mapya ya milele’ (Sura ya Ishirini na mbili). Katika sura hizi zote, mwandishi ametumia marejeo ya Biblia kama rejea yake kuu ya kihistoria na jumbe zote za kuelimisha. Mwandishi amefanya nukuu mbalimbali kutoka kwenye maandiko ya Biblia ili kukuwezesha kuelewa zaidi misingi ya elimu utakayoipata ndani ya kitabu hiki, na zaidi sana, kitabu hiki kimetumia zaidi lugha/Kiswahili cha ki-Biblia ili kuzidi kuzielekeza fikra zako kupata mafafanuzi ya kina.
Kitabu hiki kitafanyika kuwa nguzo, msaada na jibu la baadhi ya maswali yako ambayo umekuwa ukijiuliza kwa muda mrefu. Ni matumaini yangu kuwa kitakufunza na kitakupa wasaa wa kufanya tathmini ya kina ya maisha yako kama moja ya wanafunzi wa Neno la Mungu. Uwapo na maswali, mrejesho ama mawazo ya aina yoyote, nakushauri usiache kuwasiliana na Mwandishi kupata maelezo ya kina.
Kitabu hiki chafaa kwa watu wote
wanaoishi sasa na watakaokuwapo katika
nyakati zijazo.