Kanuni 21 za Kibiblia Kuhusu Utoaji
Somo la utoaji ni moja ya masomo muhimu kabisa katika Ukiristo. Imani yetu imejengwa juu ya msingi wa utoaji. Mungu wetu ni mtoaji na utoaji ni moja ya tabia yake. Maisha ya utoaji yanadhihirisha Ukiristo halisi. Katika utoaji ndipo tunapoweza kuakisi na kushiriki katika sifa na tabia ya Mungu ya upendo.
Mungu ni mtoaji na kama yeye ni lazima na sisi kuwa tuwe watoaji. Kila mtu anaweza kutoa akiamua. Kutoa ni moyo zaidi kuliko vitu unavyotoa. Hivyo upendo unapaswa kuwa ndio kisababisho kikuu nyuma ya kutoa kwetu.
Moja ya sababu ya kwa nini tunamtolea Mungu ni kwamba, tunatoa kwasababu tumepokea vingi na neema ya Mungu ni tele na nyingi sana katika maisha yetu.
Utoaji ni fursa ya kushiriki katika kazi ya Ufalme na kumtumikia Mungu kwa moyo wa furaha. Katika utoaji Mungu anatupa fursa ya kuwa mawakala wake wa mabadiliko katika ulimwengu.
Mungu anamiliki kila kitu, vitu vyote vinatoka kwake na sisi na vyote tulivyonavyo ni mali ya Mungu. Tunatoa kwa sababu sisi ni mali ya Mungu na mawakili wa vyote alivyotupatia.