Kiongozi wa Kiroho
KIONGOZI WA KIROHO ni kitabu ambacho kimeelezea mambo ishirini [20] ambayo kiongozi wa kiroho anatakiwa kuwa nayo ili aweze kuwaongoza watu sawasawa na mapenzi ya Mungu.
Ipo tofauti kubwa sana ya kiongozi wa kiroho na kiongozi wa kisiasa. Kiongozi wa kiroho anamwamkilisha Mungu kwa watu anaowaongoza. Hivyo ni lazima awe karibu na Mungu ili aweze kupokea maelekezo ya namna ya kuwaongoza watu.
Kiongozi huyu wa kiroho anatakiwa kuwa na tunu za kimungu ili awafikishe watu kwenye nchi ya ahadi. Nje ya hapo, kiongozi huyu anaweza kuwapeleka watu mahali ambapo si mpango wa Mungu.
Neno la Mungu linasema, “Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake watatumbukia shimoni wotw wawili.” [Mathayo 15:14]
Kumbe kiongozi akiwa kipofu ana nafasi kubwa sana ya kuwapeleka wengine shimoni. Kiongozi wa kiroho anapaswa kuwa mwaminifu, mwenye kupokea ushauri wa watu wengine, mwenye maono, mnyenyekevu, ambaye yupo tayari kuacha alama itakayokumbukwa na awe tayari kuwaunganisha watu anaowaongoza na Mungu wao. Asiwe mwenye kutafuta maslahi yake binafsi.