Kusifu na kuabudu katika Roho na kweli
Ibada (Kuabudu) imekuwa agenda kuu kutoka kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo kwa sababu MUNGU aliyeumba vitu vyote na kutukomboa katika Kristo YESU anastahili kupokea sifa, ibada na heshima zote (Kutoka 15: 1 - 18, Ufunuo 4:11). Hata hivyo, kwa kuwa kuna namna fulani ya ibada haikubaliki kwa MUNGU (Mwanzo 4:3 – 5, Ufunuo 9:20 – 21), ni muhimu kwetu kujua ni nini kinachompendeza MUNGU na jinsi anavyotaka tuwasilishe ibada zetu mbele zake. Mambo ambayo amefunua katika Maandiko Matakatifu yanapaswa kuwa msingi thabiti wa viwango vya ibada yetu kwa Mwenyezi MUNGU.
Watu wengi ambao ni jamii ya Waamini hudhani kuwa viongozi wa vikundi vya kusifu na kuabudu au waimbaji pekee ndio wanaopaswa kuelimishwa kwa habari ya kusifu na kuabudu. Mwandishi wa kitabu amekusudia msomaji kupata kujua umuhimu wa Kanisa lote kama mwili wa Kristo kuwa na ufahamu wa ibada ya sifa na kuabudu.
Kuabudu katika roho na kweli ni sentesi iliyotokana na mazungumzo kati ya Bwana YESU na Mwanamke Msamaria yaliyofanyika kando ya kisima.
Yohana 4:23-24 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. MUNGU ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.
Biblia inaposema Baba anawatafuta waabuduo halisi inamaanisha kuwa hao Watu ni wachache, swali la msingi kuwa je ungependa kuwa sehemu ya hao wachache wanaotafutwa na MUNGU? Kupitia mafundisho ya kitabu hiki msomaji atafanyika kuwa Mtu anayetafutwa na MUNGU hivyo mahusiano yako na MUNGU yataimarishwa.